Genesis 23

Kifo Cha Sara

1Sara aliishi akawa na umri wa miaka mia na ishirini na saba. 2 aSara akafa huko Kiriath-Arba (yaani Hebroni) katika nchi ya Kanaani, Ibrahimu akamwombolezea na kumlilia Sara.

3 bNdipo Ibrahimu akainuka kutoka pale penye maiti ya mke wake. Akazungumza na Wahiti, akasema, 4 c“Mimi ni mpitaji na mgeni miongoni mwenu. Niuzieni sehemu ya ardhi yenu ili niweze kumzika maiti wangu.”

5Wahiti wakamjibu Ibrahimu, 6 d“Bwana, tusikilize. Wewe ni mtawala mkuu sana miongoni mwetu. Zika maiti wako katika kaburi unalolipenda kati ya makaburi yetu. Hakuna mtu wa kwetu atakayekuzuia kaburi lake ili kuzika maiti wako.”

7Ibrahimu akainuka na akasujudu mbele ya wenyeji wa nchi, yaani Wahiti. 8Akawaambia, “Kama mnaniruhusu kumzika maiti wangu, basi nisikilizeni mkamsihi Efroni mwana wa Sohari kwa niaba yangu 9 eili aniuzie pango la Makpela, lililo mali yake, nalo liko mwisho wa shamba lake. Mwambieni aniuzie kwa bei kamili atakayosema ili liwe mahali pangu pa kuzikia miongoni mwenu.”

10 fEfroni Mhiti alikuwa ameketi miongoni mwa watu wake, akamjibu Ibrahimu mbele ya Wahiti wote waliokuwepo katika lango la mji. 11 g“La hasha, bwana wangu, nisikilize, nakupa shamba, pia nakupa pango lililomo ndani yake. Nakupa mbele ya watu wangu. Uzike maiti wako.”

12Ibrahimu akasujudu tena, mbele ya wenyeji wa nchi, 13akamwambia Efroni wale watu wakiwa wanasikia, “Tafadhali nisikilize. Nitakulipa fedha za hilo shamba. Kubali kuzipokea ili niweze kumzika maiti wangu.”

14Efroni akamjibu Ibrahimu, 15 h“Nisikilize, bwana wangu, thamani ya ardhi hiyo ni shekeli 400 za fedha,
Shekeli 400 za fedha ni sawa na kilo 4.5.
lakini hiyo ni nini kati yako na mimi? Mzike maiti wako.”

16 jIbrahimu akakubali masharti ya Efroni, akampimia ile fedha aliyotaja masikioni mwa Wahiti: Shekeli 400 za fedha kulingana na viwango vya uzito vilivyokuwa vikitumika wakati huo na wafanyabiashara.

17 kHivyo shamba la Efroni huko Makpela karibu na Mamre, yaani shamba pamoja na pango lililokuwamo, nayo miti yote iliyokuwamo ndani ya mipaka ya shamba hilo, vilikabidhiwa, 18 lkwa Ibrahimu kuwa mali yake mbele ya Wahiti wote waliokuwa wamekuja kwenye lango la mji. 19 mBaada ya hayo Ibrahimu akamzika Sara mkewe kwenye pango ndani ya shamba la Makpela karibu na Mamre (huko Hebroni) katika nchi ya Kanaani. 20Hivyo Wahiti wakamkabidhi Ibrahimu shamba pamoja na pango lililokuwa humo kuwa mahali pa kuzikia.
Copyright information for SwhKC